Shairi: Umbo Langu

MTUNZI KHAMIS OMAR MWINYIKAI
 
Kila ukipata shari, ni heri utunze moyo
Simanzi sikuathiri, yaka simama mamboyo
Bora uweke nadhiri ,utapata fanikiyo
Subira huvuta heri, itafika nafasiyo
 

Kando kamwe sijibari, kisa una jakamoyo
Piga chako we kidari, usiangue kiliyo
Mtegemee jabari, sijitiye bambaliyo
Subira huvuta heri, itafika nafasiyo
 

Katu mambo sikahiri, wala kufanya tishiyo
Yafanye tu kwa kadiri, tatulia imaniyo
Ya watu si kuathiri, ikaruka akiliyo
Subira huvuta heri, itafika nafasiyo
 

Kijicho kisikithiri, kukodolea wenziyo
Macho yako yasitiri, uihifadhi wenzayo
Ya watu sikuathiri, ikaruka akiliyo
Subira huvuta heri, itafika nafasiyo
 

Ulimi nakushauri ,usiseme ya wenziyo
Uchunge usikufuri ,kaiponza nafsiyo
Ukalichimba kaburi, usijuwe hatimayo
Subira huvuta heri, itafika nafasiyo
 

Mola ameshakariri, yuko na wasubiriyo
Hakika ukisubiri, takuwa shwari mamboyo
Hutakuwa na la wari, tanyooka maishayo
Subira huvuta heri ,itafika nafasiyo
 

Wako wapi wenye ari, lo fanya pupa mamboyo
Wajiona majabari, wakadunisha wenziyo
Sasa wao ni stori, kila mtu apigiyo
Subira huvuta heri ,itafika nafasiyo
 

Ya heri nakushauri, subiria nafasiyo
Aibu takuwa siri, sipo taka shauriyo
Hebu we ndugu subiri, napunguza harakayo
Subira huvuta heri ,itafika nafasiyo
 
MTUNZI KHAMIS OMAR MWINYIKAI