Shairi: Umbo Langu

Mtoto alo mrembo, mimi nimejionea

Zuri mno lakwe umbo, hakika lasisimua

Kapewa yote mapambo, ya uke ametimia

Dada nakupa hongera, kwa umbo ulilopewa

 

Mtoto alo simani, kidosho mejipatia

Umbile la wastani, salim najivunia

Nimfananishe na nani, katika hini dunia

Dada nakupa hongera, kwa umbo ulilopewa

 

Usowe unavyomwaka, mithili ya qamaria

Macho makubwa yamweka, meupe ya kulegea

Utazimia hakika anapokuangalia

Dada nakupa hongera, kwa umbo ulilopewa

 

Hebu nyumaye geuka, bila hofu angalia

Bodi lilivyojengeka, shakili ya dauria

Akenda lapepeteka, kushoto mara kulia

Dada nakupa hongera, kwa umbo ulilopewa

 

Kwa weupe huyu mwana, utadhani muarabu

Ana sifa nyingi sana, na uzuri wa ajabu

Za dhahiri nilonena, kwingine nacha aibu

Dada nakupa hongera, kwa umbo ulilopewa

 
Umbo Langu

Kwa Dua ninasimama, Mungu ninakuombea

Akupe maisha mema, mabaya kukwepushia

Litupendane daima, hadi mwisho wa dunia

Dada nakupa hongera, kwa umbo ulilopewa.

 

Na Khalfan Nzaka Salim