Ndio huo usiku wa kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni  umewadia.

Ni usiku ulojaa shamra shamra na mitikasi si haba.Aso na mwana aelekee jiwe;Wenyewe watakwambia.

Ni machache sana yanayofahamika kuhusu historia ya usiku huu ama wiki ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza (Fresher’s week).Ila wanahistoria wamejaribu kueleza kuwa kundi la kwanza la wanafunzi waliojiunga na chuo kikuu cha Oxford mwaka wa 1167 huenda walianzisha usiku huo.

Kuja kwa teknolojia na mitandao kukabadilisha maana na jinsi usiku huu ulivyosherehekewa.Hapo awali hakukuwa na teknolojia na wanafunzi walilazimika kukaa zaidi ya wiki moja wakijaza fomu za kujiunga na chuo.Wanafunzi wale wa mwaka wa pili hadi wa nne walokuwa wamekaa  chuoni humo  kwa muda wakaamua kuanzisha jambo ambalo lingewashughulisha wao na wale wa mwaka wa kwanza.Hapo ndipo yalipoanzia.

Baada ya muda na kuja kwa teknolojia mambo yakabadilika.

Waliopitia vyuo vikuu nchini watakuwa  washawahi jipata kwenye usiku huu wa kukata na shoka.Usiku wa ndovu kumla mwanae.kwa wale walokole na waashiki shakiki wa maadili  ya kidini wawatakuwa washaskia kuuhusu usiku huu.

Japo lengo na madhumuni ni kuwakaribisha wanafunzi wapya kwenye maisha ya chuoni,wengi wa watu hutumia nafasi hii kwa kujifaidi binafsi.Kila mwamba ngoma huvutia upande wake,eti ee!

Vileo na vinywaji Vya kila aina husheheni.Kuna wale wanaopiga pafu moja au mbili za sigara ama chochote kile kinachovutwa kupitia mdomo.Hapo vinywaji havinywewi,huogewa.Maisha yenyewe mafupi bwana wee…

Watoto wa kike wasohatia hupoteza ubikra wao  (ashakum si matusi) bila ya kutarajia.Lakini hayo si neno! Wapo wanaopata ujauzito ambao hawakuupangia.Ni yale ya mwana kuzaa mwana.

Usiku huu pesa za mikopo ya HELB hupelekwa tenge.Kilichopangiwa kutumiwa kwa muhula mzima huisha ndani ya usiku mmoja.

Wanafunzi hunywa kumwaga.Anacho kunywa ndani ya usiku mmoja hushinda kile atakachokunywa ndani ya miaka miatatu ijayo atakayobaki chuoni.Ponda mali kufa kwaja,au siyo?

Mabango hubandikwa kwenye kila kuta za chuo ,kauli mbiu ikiwa “Kosa uchekwe”.Lakini huo muda na nguvu ya kuchekwa wakosao hupatikana kweli…?Maana baada ya hapo hata kutembea ‘makomredi’ hushindwa.

Ni usiku wa “nyakua fresher” kama wawaitavo wenyewe.Chupa moja au mbili za pombe zikitosha “kunyakua” mboga mpya kama wawaitavo wasichana wa mwaka wa kwanza.

Yanayofanyika kwenye kuta na vyumba vya chuo usiku huu ni mingi.Kuta zingekuwa na mdomo zingesema.

Yote ni tisa,la kumi;kila mmoja na starehe zake.Ulazima wa kustarehe na kujiburudisha upo.Hakuna akatazwaye kujibudurudisha,ila binadamu hasa wanafunzi wa kiwango cha chuo kikuu tunafaa kujiburudisha kwa makini na tahadhari.Starehe zingine ni duni duniani.

Tandabelua la Fresher's Night